Papa Francis aomba kuzimwa kwa milio ya silaha kote duniani

  • VOA News

Papa Francis akitoa hotuba ya Krismasi kwenye bustani ya St Peter mjini Vatican Jumatano. (Picha ya/ VATICAN MEDIA)

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis Jumatano katika  hotuba yake ya kawaida wakati wa Krismasi amewasihi “watu wa mataifa yote” kuwa na ujasiri katika mwaka huu Mtakatifu, kwa kuzima milio ya silaha na kumaliza migawanyiko inayoikumba Mashariki ya Kati, Ukraine, Afrika na Asia.

Hotuba hiyo maalum ya Krismasi maarufu kama ‘Urbi et Orbi’ kwa kitaliano au ‘Kwa mji na Dunia’ huangazia baadhi ya masaibu yanayoikumba dunia. Krismasi ya mwaka huu imeendana na mwanzo wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa 2025 ambao amesema utakuwa wa amani, wakati akiomba maridhiano na hata adui zetu.

“Naomba kila mmoja na watu wa mataifa kuwa mahujaji wa amani, ili kunyamazisha milio ya silaha na kumaliza migawanyiko,” Papa Francis alisema kwenye bustani ya St Peter’s Basilica, mbele ya umati mkubwa wa watu.

Aliomba silaha zikomeshwe kwenye vita vya Ukraine na Mashariki ya Kati, huku pia akisisitiza kuachiliwa kwa mateka wa Israel waliotekwa na Hamas Oktoba 7, mwaka jana.