Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara atangaza serikali yeke

Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara, alipoapishwa rasmi mjini Abidjan kuwa Rais wa nchi hiyo Mei 6, 2011

Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara ametangaza serikali yake ya kwanza tangu achukue madaraka baada ya miezi kadhaa ya uchaguzi uliokuwa na mzozo mkubwa.

Rais Ouattara amewateuwa mawaziri 36 jana Jumatano, lakini hakuwajumuisha wanachama wowote kutoka chama cha Rais wa zamani Laurent Gbagbo, ambaye alikataa kujiuzulu baada ya uchaguzi wa mwezi Novemba.

Bwana Ouattara awali alisema anataka kuwajumuisha maofisa kutoka pande zote zenye mzozo. Hata hivyo, maafisa kutoka chama cha bwana Gbagbo wamesema hawawezi kujiunga na serikali ambayo imemtia ndani bwana Gbagbo.

Watu wasiopungua 3,000 waliuwawa katika ghasia za baada ya uchaguzi wakati Rais Gbagbo ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2000, alipokataa kuyakubali matokeo ya kushindwa kwake. Hatimaye bwana Gbagbo aliangushwa na kukamatwa April 11, baada ya helikopta za Umoja wa Mataifa na Ufaransa kulipopiga eneo la makazi ya rais mahali alipokuwa amejificha.

Makundi ya haki za binadamu yanawashutumu wafuasi wa viongozi wote bwana Ouattara na bwana Gbagbo kwa mauaji na kuwajeruhi raia katika mapigano ya kuwania madaraka. Rais Ouattara ameahidi haki kwa waathirika wote wa ghasia hizo.