Upinzani DRC wapinga wazo la Kabila

Wafuasi wa rais Joseph Kabila wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Vyama vya upinzani huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC vinakataa wazo la raundi moja ya uchaguzi wa Rais,lililopendekezwa na Rais Joseph kabila.

Serikali ya kabila ilitoa wazo hilo wiki iliyopita ikisema hatua hiyo inapunguza uchaguzi kutoka raundi mbili hadi moja na itaokoa mamilioni ya fedha. Hata hivyo kundi moja la upinzani lilikataa wazo hilo siku ya Jumapili.

Shirika la habari la Ufaransa lilimkariri Francois Mwamba wa chama cha MLC akisema pendekezo hilo lililenga kupanga wizi, na kuruhusu mtu mmoja kushikilia madaraka yote.

DRC ni nchi kubwa yenye watu wasiopungua milioni 60, ilikumbwa na vita kwa miaka kadhaa na mgogoro wa kikabila. Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kwamba chini ya mfumo mmoja wa uchaguzi, mgombea mmoja wa urais anaweza kuwa rais kwa kushinda kiasi cha asilimia 20 tu ya kura.
Rais Kabila alichaguliwa mwaka 2006 kwa kumshinda mpinzani wake Jean-Pierre Pemba katika duru ya marudio ya uchaguzi mkuu.

Chini ya mfumo uliopo DRC inatarajiwa kufanya duru ya kwanza ya uchaguzi wa Rais mwezi Novemba na duru ya pili itafanyika mwanzoni mwa mwaka 2012 kama ikibidi. Bunge litatakiwa kupitisha mabadiliko ya katiba kuwa ya mfumo wa raundi moja ili uweze kutumika.