Akihutubia wafuasi wake katika bustani ya Jivanjee, jijini Nairobi, Odinga vile vile ametishia kuwaongoza wafuasi wake kuilazimisha serikali ya sasa inayoongozwa na rais Dr. William Ruto kuweka ruzuku kwa bidhaa muhimu kama mafuta na kupunguza kiwango cha kodi.
Anataka vile vile matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti mwaka uliopita kufanyiwa ukaguzi utakaofanywa na tume huru akidai kwamba ndiye mshindi wa uchaguzi huo. Bila kufanyika ukaguzi anaotaka, Odinga amesema kwamba “atawaongoza wafuasi wake kurejesha sauti na mamlaka yao.”
Odinga na wafuasi wake wamekusanyika katika bustani ya Jivanjee kwa msingi kwamba walikuwa wanaandaa maombi. Hafla hiyo imeonyeshwa moja kwa moja kwenye ukurasa wake wa Facebook.
“Wale ni wanafiki, kila Jumapili wanaingia kanisani kujifanya eti wanaomba, kumuamsha mungu lakini baadaye wanatenda maovu makubwa zaidi,” amesema Odinga, katika kile kimeonekana kama kumlenga rais Ruto ambaye amekuwa akiongoza maafisa katika serikali yake kwa hafla za maombi kila mara.
“Nchi yetu iko katika hali mbaya ndio sababu tunasema kwamba mwenyezi mungu pekee yake ndiye anaweza kuamua kuisaidia Kenya. Lakini biblia inasema kwamba Mungu anawasaidia wale wanaojisaidia. Viongozi wa dini wako na sisi. Wahindu, makalasinga hata viongozi wa dini za kienyeji wako na sisi. Kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta na chakula wakati kuna kiangazi ni hatua potofu na ya kutojali. Lazima ruzuku irudishwe, lazima bei ya bidhaa na kiwango cha ushuru kishuke.”
Madai ya wafuasi wa Odinga kukamatwa
Hafla hiyo ya maombi hata hivyo imejaa shutuma na shinkizo dhidi ya serikali. Amedai kwamba serikali inatumia maafisa wa polisi kuwahangaisha waliokuwa maafisa wa ngazi ya juu katika serikali ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
Shutuma hizo zimetolewa siku chache baada ya polisi kuingia nyumbani kwa aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani Dr. Fred Matiang’i katika operesheni ambayo polisi walisema ilikuwa ya kutaka video ya CCTV.
Ni tukio lililojiri baada ya Odinga na vyombo vya habari vya Kenya kudai kwamba polisi walikuwa wameingia kwa Matiang’i usiku wakitaka kumkamata.
Polisi walisema kwamba habari hizo zilikuwa za uongo na hakuna mpango wowote wa kumkamata waziri huyo wa zamani.
Polisi walisema kwamba Odinga na Matiang’i walikuwa wamepanga ‘ukamataji bandia’ ili kuzua taharuki nchini na kwamba vyombo vya habari vya Kenya vilitumiwa kupeperusha habari potofu.
Hakuna ushahidi wowote umetolewa kufikia sasa kuonyesha kwamba polisi walikuwa nyumbani kwa Matiang’i kwwedna kumkamata. Tukio hilo lilipelekea kuanza kwa uchunguzi na kuchukuliwa kwa video za CCTV kwa lazima kutoka nyumbani kwa Matiang’i.
Odinga sasa anadai kwamba polisi wanawahangaisha watu walio karibu naye.
“Tunaona vile wanaendelea kuwatesa wale waliokuwa katika serikali ya Uhuru. Juzi wamekwenda kumtesa Matiang’i halafu sasa wanataka kumtesa wakili Danstan Omari. Ameandikiwa barua na DCI eti wanamchunguza. Huyu ni wakili alikuwa anafanya kazi yake ya uwakili. Tunataka kuwaambia waachane na Mating’i na waachane na Danstan Omari,” amesema Odinga akisisitiza kwamba “tunawaambia hata mkitumia nguvu kiasi gani, hamtaweza kwa sababu wakenya wanakuja kwa jumla mpende msipende.”
Odinga anataka serikali kuwalinda wafuasi wake wanapoandamana.
“Tunataka Ruto na watu wake wafundishwe kwamba maandamano ya amani ni halali. Maandamano hufanyika mbele ya bunge la Uingereza. Hufanyika mbele ya ikulu ya Marekani. Hufanyika mbele ya bunge la Marekani. Maandamano ya amani yanaruhusiwa na waandamanaji wanasindikizwa na polisi.”
Tume huru ya mipaka na uchaguzi IEBC
Kwa mara nyingine tena, Odinga anataka mchakato wa kujaza maafisa wa tume huru ya mipaka na uchaguzi IEBC, waliostaafu na kujizulu, kusitishwa mara moja, akisema kuna upendeleo na unafanywa na mtu mmoja.
Vita kati ya Odinga na tume ya uchaguzi ni vya muda mrefu tangu mwaka 1997 alipogombea urais kwa mara ya kwanza, wakati wa utawala wa hayati Daniel Arap Moi.
Baadaye aliitisha maandamano dhidi ya tume ya uchaguzi wakati wa utawala wa hayati Mwai Kibaki na wakati wa utawala wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
licha ya mabadiliko yanayofanyika kila mara anapotaka mabadiliko hayo, huitisha maandamano na mabadiliko mengine katika tume hiyo baada ya uchaguzi mkuu, na kushindwa au kudaiwa kuibiwa ushindi katika kila uchaguzi anaoshiriki kugombea urais.
Raila Odinga aligombea urais kwa mara ya 5 mwaka uliopita 2022 bila mafanikio.
Ruto amjibu Raila
Akizungumza wakati wa kuzindua jopo maalum la kuusafisha mto Nairobi, katika mtaa wa Korogocho, Nairobi, rais William Ruto amemjibu Raila akisema kwamba serikali yake haiwezi kutishwa na watu wanaoiwekea masharti.
Hotuba ya rais Ruto imepeperushwa moja kwa moja kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Amesema kwamba gharama ya Maisha itashuka pole pole lakini sio ndani ya siku ambazo Odinga na wanasiasa wenzake wa upinzani wanataka.
“Ati wanataka kututisha na maandamano, watafanya maandamano hadi watachoka. Kila mtu lazima aheshimu sheria na nchi hii inaongozwa na sheria na tutahakikisha kwamba kila mtu anaheshimu katiba.” Amesema Ruto akiongezea kwamba “Nataka kuwaambia Rafiki zangu ambao wamezoea kuvunja sheria, ambao wamezoa kulazimisha mambo yao kufanyika kwamba hii ni nchi itakayoongozwa kwa kuheshimu sheria na hakuna atakayewatisha wakenya.”
Ruto amemshutumu Raila akidai kwamba ndiye aliyechangia kuongezeka kwa gharama ya maisha Kenya wakati alipoingia katika serikali kwa kile kinachojulikana kama ‘salamu na Kenyatta’ yani ‘handshake’.
“Ulikuwa na miaka 5, bei ya unga ilipanda hadi shilini 230. Tumepunguza hadi shilingi 180. Watupatie muda na bei ya unga itashuka hadi shilingi 140.” amesema Ruto akiongezea kwamba "walituacha na madeni mengi karibu nchi yetu iteleze iingie mahali ambapo ingekwama. Saa hizi tumeanza kupunguza madeni. katika bajeti ya mwaka huu tumepunguza bilioni 300 ya madeni hata wale walikuwa wametufungia katika masoko ya kimataifa, katika mashirika ya fedha ya kimataifa, hata kiwango cha riba ambacho kilikuwa kimefikia asilimia 17 tumeteremsha na kufika chini ya asilimia 10 kwa soko la kimataifa."
Kuhusu tume ya uchaguzi, Ruto amemjibu Raila akisema, “Mambo ya viongozi na uchaguzi tulimaliza mwezi wa nane. Ile kazi tumehakikisha sasa ni ya wananchi hawa. 2027 ni miaka 5 ijayo, sasa tunataka kuongelea mambo ya hawa wananchi ya leo, ya kesho na kesho kutwa mpaka ifike siku hiyo.”