Pia Odinga anamshutumu Ruto kuendelea kuunda upya tume ya uchaguzi bila mashauriano na kushindwa kuondoa ushuru wa ziada kwa bidhaa muhimu.
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ametangaza rasmi kuanza kampeni ya maandamano ya amani kote nchini humo dhidi ya serikali ya Rais William Ruto kwa kushindwa kupunguza gharama ya juu ya maisha, kuendelea kuunda upya tume ya uchaguzi bila mashauriano na kushindwa kuondoa ushuru wa ziada kwa bidhaa muhimu.
Odinga alimtaka rais Ruto, katika kipindi cha siku 14, kurejesha ruzuku ya chakula, mafuta na elimu pamoja na kufungua seva za uchaguzi wa urais wa 2022 lakini amehindwa kufanya hivyo.
Baada ya kumalizika kwa muda huo uliotolewa wa siku kumi na nne, Alhamisi, Bw Odinga amesisitiza kuwa utawala wa Ruto sasa utahitajika kukabiliana na hasira za umma utakaoshiriki kampeni ya kuikaidi serikali yake kupitia maandamano ya amani, kugoma kwa aina mbalimbali na hata kuingia afisi za umma kutaka majibu.
Odinga, anasema Ruto ameshindwa kushusha gharama ya maisha, kuondoa ushuru unaolemaza ufikiaji wa bidhaa za msingi, na kujikita katika harakati za kubuni upya tume ya uchaguzi IEBC baada ya makamishna wanne kufukuzwa kazi.
Aidha, Odinga anaeleza kuwa uamuzi wa serikali ya rais Ruto kuondoa marufuku ya uzalishaji na uagizaji wa vyakula vilivyofanyiwa mabadiliko ya kigenetiki, maarufu kama GMO, ulioidhinishwa na Baraza la Mawaziri kuruhusu uingizaji wa mazao ya kibayoteknolojia ili kuifanya Kenya kujitosheleza kwa chakula na kudhibiti bei ya bidhaa za msingi, utawaumiza wakulima wa ndani na kuongeza njaa.
Odinga, kando na kudai kuwa mahakama za Kenya zimetekwa na utawala wa rais Ruto, ameendelea kukariri kuwa hatua ya Ruto kuondoa ruzuku kwa chakula na elimu wakati taifa linakabiliana na ukame mbaya sana na baa la njaa kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miongo minne, ni kutojali na kutokuwa na moyo wa huruma kwa raia wa Kenya.
Baada ya kushika hatamu za uongozi kufuatia ushindi wake wa uchaguzi wa Agosti 9, Rais Ruto aliondoa kabisa ruzuku iliyokuwa imewekwa na rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwenye bidhaa kama vile mafuta, unga wa mahindi na umeme, iliyokuwa ikiwakinga raia dhidi ya gharama ya juu ya maisha akionya kuwa hali hiyo haikuwa na uendelevu wowote, na badala yake akaeleza kuwa ataendelea kuwekeza kwenye mikakati ya kuboresha uzalishaji wa chakula cha kutosheleza mahitaji ya umma.
Makamu wa rais wa zamani na kiongozi wa chama cha Wiper Democratic Kalonzo Musyoka, ameeleza kuwa utawala wa rais Ruto umeanza kuonyesha dalili za ukandamizaji wa uhuru na kutangaza maandamano na ususiaji huu, utakuwa wa manufaa kwa mafanikio ya demokrasia nchini Kenya.
Awali, Ruto alipuuza shinikizo la upinzani la kufanya maadamano lakini je, anajikuta katika hali gani baada ya tangazo la Odinga? Mark Bichache, mfuatiliaji wa siasa za Kenya, anadadisi.
Odinga anayeendelea kudai kuwa ndiye mshindi wa kura ya urais na kutaka seva za tume ya uchaguzi anazodai zilidukuliwa na kufanyiwa ulaghai na mfumo wa teknolojia wa tume hiyo ukaguliwe, alikuwa amempa rais Ruto makataa ya siku 14 la sivyo awaamrishe wafuasi wake kushiriki maandamano.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera, Kenya.