Marekani kuongeza msaada kwa Iraq

Rais Obama atowa ahadi ya msaada zaidi kwa Iraq


Rais Barack Obama wa marekani aliahidi Jumanne msaada wa kibinadamu wa takriban dola milioni 205 kwa Iraq, lakini hakusema lolote hadharani kuhusu kuongeza msaada wa silaha na wanajeshi uliokuwa umeombwa na waziri mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi.

Baada ya mkutano baina ya viongozi hao wawili hapo White House, Bw. Obama alisema kwamba vikosi vya Iraq vimepata vifaa na ujuzi zaidi tangu Bw. Abadi alipochaguliwa kuwa waziri mkuu nchini Iraq miezi 7 iliyopita na kadhalika msaada wa mashambulizi ya anga kutoka kwa vikosi vya marekani,vilosaidia kuteka tena takriban robo ya eneo lililoshikiliwa na wanamgambo wa Islamic State.

Rais Obama na Waziri Abadi pia walizungumzia swala la kuhusika kwa Iran kwenye mapigano dhidi ya Islamic State nchini Iraq Bw. Obama akisema kuwa nchi hizo mbili ni majirani na ni vyema kuwa na uhusiano mwema lakini akahimiza kwamba opersheni zote za kijeshi nchini humo lazima ziongozwe na jeshi la Iraq.