Obama kufanya mkutano na Raul Castro

Rais Obama akisalimiana kwa mkono na rais Raul Castro wa Cuba Aprili 10, 2015

Katika ufunguzi wa kongamano la mabara ya Amerika Ijumaa, rais Obama na rais Castro walisalimiana kwa mikono, hatua inayoashiria juhudi za kuzika uhasama wa miongo kadhaa baina ya Marekani na Cuba.

Rais wa Marekani Barack Obama na rais wa Cuba Raul Castrol wanatazamiwa kuweka rekodi ya kihistoria Jumamosi watakapofanya mkutano wa ana kwa ana, kando kando ya kongamano la mabara ya Amerika nchini Panama.

Mazungumzo hayo ya ana kwa ana yatakuwa ya kwanza kati ya viongozi wa Marekani na Cuba tangu mwaka wa 1956 na yanafanyika baada ya marais hao wawili kutangaza mwezi Desemba kurejesha mahusiano kati ya nchi zao mbili.

Katika ufunguzi wa kongamano hilo jana Ijumaa, bwana Obama na bwana Castro walisalimiana kwa mikono, hatua inayoashiria juhudi za kuzika uhasama wa miongo kadhaa baina ya nchi zao mbili.

Kuna taarifa zisizothibitishwa kuwa katika mkutano wa Jumamosi huenda rais Obama akatangaza kuiondoa Cuba kwenye orodha ya nchi zinazodhamini ugaidi.

Cuba imeomba kuondolewa kwenye orodha hiyo, ikisema ni kikwazo ambacho kimezuia majadiliano ya kurejesha mahusianio ya kidplomasia baina ya Marekani na Cuba.