Obama ataka biashara zaidi na India

Rais Barack Obama akizungumza huku Mkurugenzi wa Mahindra & Mahindra Ltd. Anand Mahindra akisikiliza wakati wa mkutano na wafanyabiashara.

Rais Obama atangaza mipango ya kupunguza masharti ya biashara na India kuinua biashara kati yao.

Rais Barack Obama wa Marekani ametangaza mipango ya kupunguza masharti ya biashara na India katika juhudi za kuinua uhusiano wa kibiashara na nchi hiyo inayoinukia kwa nguvu za kiuchumi. Rais obama alitangaza hatua kadha kupunguza masharti ya kupeleka bidhaa India katika hotuba aliyotoa Jumamosi mbele ya kundi la wafanyabiashara wa Marekani na India katika mji wa Mumbai ambao ni kituo kikuu cha kifedha.

Bw Obama pia alielezea makubaliano kadha ya biashara na India ambayo anasema itafungua nafasi za kazi elfu 54 nchini Marekani.

India ni kituo cha kwanza katika ziara ya siku 10 ya rais Obama huko Asia. Rais Obama na mkewe wanakaa katika hoteli ya Taj Mahal mjini Mumbai ambayo ilishambuliwa na magaidi Novemba 2008 ambapo watu 166 waliuawa. Katika hotuba yake alisema hoteli hiyo ni "ishara ya nguvu na uvumilivu wa watu wa India" dhidi ya magaidi.

Waandika makala wa India walionyesha kusikitikishwa kwamba rais Obama hakuitaja Pakistan katika hotuba yake kuhusu mashambulizi ya Mumbai kwa sababu ya madai kuwa washambuliaji hao walitokea Pakistan. India inalilaumu kundi la Pakistan la Lashkar-e-Taiba kwa mashambulizi hayo.