Maandamano hayo, ambayo yamekuwa yakiongozwa na kizazi maarufu kama Gen-Z, wakati yakirushwa moja kwa moja kwenye majukwaa ya kimitandao, hayakutarajiwa na serikali, huku taharuki kuhusu sera za kiuchumi za Ruto ikiongezeka. “Vijana wetu wamejitokeza na kuangazia masuala yanayohusu taifa lao. Wametekeleza jukumu lao la kidemokrasia na ni hatua ya kujivunia,” amesema Ruto kulingana na msemaji wa ofisi ya Rais Hussein Mohamed kupitia ukurasa wa X.
Tayari watu wawili wamekufa huku wengine wengi wakijeruhiwa wakati wa maandamano hayo kwenye mji mkuu wa Nairobi, kwa mujibu wa watetezi wa haki. Maandamano hayo yalianza Nairobi Jumanne, kabla ya kuenea kwenye miji mingine kote nchini, wakati waandamanji wakiitisha maandamano ya kitaifa Jumanne Juni 25. Utawala wa Ruto umetetea hatua ya kuongeza ushuru, ukidai kuwa itaongeza kipato cha serikali, pamoja na kuzuia utegemezi wa mikopo kutoka nje.