Rais-mteule wa Marekani Donald Trump amemteua Gavana wa jimbo la South Carolina, Nikki Haley Jumatano kuwa balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa.
Nikki mwenye umri wa miaka 44, mtoto wa kike wa wazazi wahamiaji kutoka India anahudumu muhula wa pili kama gavana, lakini hana uzoefu wa sera za kigeni.
Amekuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa katika baraza la mawaziri la Trump ambalo limejaa wanaume. Haley hakumuunga mkono Trump wakati wa kampeni zake za muda mrefu za kuwania urais. Awali alimuunga mkono seneta wa Florida, Marco Rubio na wakati alipojitoa kwenye kinyang’anyiro cha urais, alielekeza uungaji mkono wake kwa seneta wa Texas, ted Cruz.
Muda mfupi kabla ya uchaguzi mkuu wa Novemba nane, alisema kwamba hakuwa na hamasa kuhusu chaguo la mgombea anayewania kuingia Ikulu ya Marekani, wakati Rais Barack Obama anapomaliza muda wake madarakani mwezi Januari, na kwamba atampigia kura Trump.