Nigeria yerejesha raia wake kutoka Saudi Arabia

Watu wakitembea kwenye barabara za Abuja,Nigeria

Nigeria Alhamisi imewarejesha mamia ya raiya wake waliokwama Saudi Arabia baada ya kupitisha muda wa vibali vyao vya kuishi huko.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, ndege ya kwanza iltua mjini mkuu wa Abuja wakati watu wakiwa wamejifunika kwa barakoa na kuvaa magwanda marefu.

Ukosefu wa ajira pamoja na hali ngumu ya kiuchumi nchini Nigeria katika kipindi cha miaka minne iliopita, vimepelekea maelfu wa wanigeria kutafuta ajira kwenye mataifa ya kigeni.

Hata hivyo janga la corona limesababisha upungufu wa ajira kwenye mataifa mengi huku mengine yakiongeza kanuni ya usafiri zilizopelekea wengi wao kukwama.

Video iliokuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ilionyesha wanaigeria wanaodai kushikiliwa kwenye kambi moja ya Saudi Arabia kwa zaidi ya miezi tatu, wakati mataifa mengine yakisemekana kuchukua raiya wake baada ya takriban wiki mbili.

Serikali ya Nigeria ilisema Jumatatu kuwa ilikuwa ikishauriana na Saudi Arabia kuhusu kuwarejesha raiya wake 802 kwa kutumia ndege mbili Alhamisi na Ijumaa.