Wanigeria wajitokeza kwa wingi kupiga kura

WaNigeria wakisubiri kupiga kura leo March 28.

Wananchi wa Nigeria walijitokeza kwa wingi Jumamosi March 28 kupiga kura katika uchaguzi wa rais na bunge baada ya kucheleweshwa kwa wiki sita kwa sababu ya vitisho vya magaidi wa Boko Haram.

Upigaji kura ulianza Jumamosi mchana baada ya wananchi kutumia muda wa asubuhi kukamilisha uandikishaji huku kukiwa na ripoti za mashambulizi katika baadhi ya maeneo ya nchi. Watu wanaoshukiwa kuwa Boko Haram walishambulia katika majimbo ya Gombe na Bauchi, kaskazini ya Nigeria wakitisha watu wasijitokeze kupiga kura.

Vituo vingi vya kupigia kura vilichelewa kufunguliwa kutokana na upungufu wa vifaa lakini wananchi walifanya subira sehemu nyingi kupiga kura zao.

Rais Goodluck Jonathan ambaya anapambana na kiongozi wa zamani wa kijeshi Muhammadu Buhari alilazimika kusubiri nusu saa nzima kabla ya kupiga kura na akatoa wito kwa wanigeria kuwa subira na kupiga kura kwa amani.