Milipuko ya mabomu yasababisha vifo nchini Nigeria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, akisalimiana na mgonjwa mmoja katika hospitali ya Abuja nchini Nigeria.

Mifululizo ya milipuko ya mabomu ndani ya kantini moja maarufu ndani ya kituo cha jeshi huko kaskazini mwa Nigeria, Jumapili usiku iliwauwa watu wasiopungua 10 na kuwajeruhi zaidi ya 20 wengine.

Kamishna wa polisi katika jimbo la Bauchi, Mohammed Abdulkadir Indabawa, alisema milipuko ilitokea kwenye soko la Mamy ambalo lilikuwa limefurika umati wa watu.

Katika tukio tofauti huko Zuba pembeni ya mji mkuu Abuja, kulitokea mlipuko mdogo kwenye kibanda cha kuuzia bia, lakini hakuna majeruhi mahututi walioripotiwa. Hakuna yeyote aliyedai kuhusika na milipuko hiyo.

Ghasia zilitokea saa chache baada ya kuapishwa kwa Rais Goodluck Jonathan ambaye alikula kiapo cha kushika madarakani jana Jumapili.

Katika hotuba yake baada ya kuapishwa kiongozi huyo mpya wa Nigeria aliahidi kupambana na rushwa na kuboresha elimu na nafasi za ajira nchini humo, pamoja na kupigania demokrasia kote barani Afrika.Alisema anawakilisha matumaini ya wa-Nigeria wote.

Rais Jonathan alisema pia ana mipango wa kufanya mageuzi katika sekta ya taifa ya mafuta nchini humo na kuimarisha mpango wa msamaha kwa wanamgambo wa zamani katika jimbo lenye utajiri wa mafuta la Niger Delta.

Bwana Jonathan aliingia madarakani mwaka jana kufuatia kifo cha kiongozi wa zamani nchini humo, Umaru Musa Yar’Adua. Alichaguliwa kiongozi mpya wan chi hiyo mwezi uliopita katika uchaguzi ambao upinzani unasema uligubikwa na wizi wa kura.