Niger yataka kujadili kuondoka kwa Ufaransa nchini humo

Viongozi wa mapinduzi ya Niger, wanataka kujadili juu ya mpango wa jinsi  mkoloni wake wa zamani Ufaransa, ataondoa wanajeshi wake nchini humo, jambo ambalo Paris, inasema itamalizika mwishoni mwa mwaka.

Utawala huo mpya umesema katika taarifa kupitia televisheni ya taifa Jumatatu kwamba muda uliopangwa wa kujiondoa lazima uwe umewekwa kulingana na makubaliano na uwe wa muafaka wa pamoja.

Imefikia takriban miezi miwili toka kuondolewa madarakani rais wa Niger, aliyechaguliwa kidemokrasia Mohamed Bazoum, hapo Julai 26.

Siku ya Jumapili, rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, alitangaza kwamba Paris itamuondoa balozi wake kutoka Niger, na kufuatiwa na majeshi ya Ufaransa katika miezi kadhaa ijayo yote yakiwa ni mahitaji ya utawala baada ya mapinduzi ya Niamey.