Wanamgambo wanaoshukiwa kuwa wa kundi la Boko Haram waliwaua kwa risasi wakulima 11 kusini mashariki mwa Niger, tisa kati yao ni kutoka Niger na wawili kutoka Nigeria, meya wa mji jirani na mahala shambulio limetokea amesema leo Jumatano.
Issa Bonga, meya wa mji huo kulikofanyika shambulio hilo, ameiambia AFP kwamba “ Wakulima 11 waliuawa kwa kupigwa risasi Jumanne na wapiganaji wa Boko Haram, umbali wa kilomita 7 kutoka mji wa Toummour.”
Meya huyo amesema waathirika hao walikuwa wameenda kukata kuni msituni.
Mji huo unapatikana katika jimbo la Diffa karibu na bonde la ziwa Chad, ni eneo muhimu kijeshi, ambako mipaka ya nchi nne ambazo ni Cameroon, Chad, Niger na Nigeria inakutana.
Boko Haram na hasimu wake, kundi la Islamic State in West Africa Province (ISWAP), waliweka ngome zao katika visiwa vingi vidogo katika bonde kubwa la bonde la ziwa Chad.