Ni uhaini kumuapisha rais mbadala Kenya - mwanasheria mkuu

Mwanasheria mkuu wa Kenya, Githu Muigai (katikati)

Mwanasheria mkuu wa Kenya Githu Muigai, alisema alhamisi kwamba ni uhaini wa hali ya juu kwa mtu yeyote kuapishwa kama rais wa nchi hiyo iwapo tayari kuna rais ambaye ameapishwa kwa mujibu wa katiba.

Muigai alikuwa akijibu tetesi kwamba kiongozi wa muungano wa upinzani wa Kenya, Raila Odinga, ataapishwa kama "rais wa wananchi' mnamo tarehe 12 Disemba.

Mwanasheria huyo aliwaambia waandishi wa habari mjini Nairobi kwamba sheria za uhalifu nchini Kenya ziko bayana kuhusu hatua zinzofaa kuchukuliwa kwa mtu yeyote atakauevunja sheria hiyo.

"Hakuna mtu mwingine aliye na mamlaka ya utawala wa nchi isipokuwa kama inavyoelezwa kwa katiba ya Kenya," alisema Muigai.

"Adhabu ya uhaini nchini Kenya ni kifo," aliongeza.

Aidha aliongeza kwamba hatua ya Muungano wa upinzani, NASA, wakutaka kuundwa kwa bunge la wananchi ni kinyume cha sheria.

Msemaji wa serikali Eric Kiraithe aliongeza kwamba katiba ya Kenya imempa mamlaka rais wa sasa kikamilifu na yeyote atakjayevunbja sheria, atakabilianwa naye ipasavyo.

Kwa upande wake NASA imeendelea kusisitiza kwamba haitambui urais wa Uhuru Kenyatta na kwamba ni sharti mageuzi yafanyike kwa mfumo wa uchaguzi kabla ya uchaguzi mwingine "huru na wa haki' kufanyika nchini humo.

Odinga alijitoa kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi wa marudio ulioitishwa na tume ya uchaguzi na mipaka (IEBC) baada ya mahakama ya juu kubatilisha uchaguzi wa tarehe nane mwezi Agosti.