Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alirejea nchini kwake kutoka Marekani na kutishia haraka kulipiza kisasi kwa shambulizi kutoka Lebanon ambalo limeua watoto na vijana 12 wa Druze.
Ilikuwa ni idadi kubwa zaidi ya vifo kutokana na shambulio la Hezbollah dhidi ya Israel toka vita dhidi ya Hamas kuanza mwezi Oktoba.
Netanyahu amekatisha safari yake ya Marekani kwa saa chache ili arejee Israel. Amesema Israel italipiza kisasi kwa shambulizi la Hezbollah lililoua watoto na vijana 12 waliokuwa wakicheza soka katika kijiji karibu na mpaka na Lebanon.
Amesema taifa la Israel halitaacha shambulizi hili lipite hivihivi.
“Wengi nchini Lebanon walikuwa wanatazamia jibu la Israeli. Maelfu ya Walebanon kusini mwa nchi hiyo walikimbia makazi yao wakihofia mashambulizi ya Israel. Hezbollah ilikanusha kuwa ilihusika, lakini Marekani na Israel zilisema hakuna shaka.”
Msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari alisema haya.
“Taasisi ya kigaidi ya Hezbollah ilirusha roketi kwa watoto wanaocheza katika uwanja wa soka wa Majdal Al-Shams kaskazini mwa Israel, Hezbollah kisha wakaudanganya ulimwengu wote na kudai kuwa hawakufanya shambulizi hilo. Huu ni uongo, na tunaweza kuthibitisha kwamba Hezbollah iliwauwa watoto 10 katika shambulizi hilo la kikatili.”
Idadi ya waliofariki baadaye iliongezeka na kufikia 12.
Wadruze ni Waarabu walio wachache ndani Israeli ambao ni raia wa Israeli. Wengi wanahudumu katika jeshi la Israeli. Maelfu ya watu walihudhuria mazishi ya watoto 12 waliouawa na kuitaka serikali ya Israel kujibu mapigo makali.
Hagari amesema shambulizi hilo linaonyesha sura halisi ya Hezbollah kama taasisi ya kigaidi.
“Kwa zaidi ya miezi tisa, Hezbollah inashambulia raia wetu kaskazini ikirusha maelfu ya makombora na UAVs kaskazini mwa Israeli, ikilenga nyumba, familia na jamii.”
Wachambuzi wa Israel wamesema Israel na Hezbollah ziko karibu zaidi kufikia vita vya pande zote kuliko ilivyokuwa toka vita kati ya Israel na Hamas vianze Oktoba 7. Toka Hezbollah ianze kurusha makombora dhidi ya Israel, taifa la kiyahudi limefanya mamia ya mashambulizi ya anga ambayo yamesababisha vifo vya watu. Walebanon 400, wakiwemo mamia ya wanachama waandamizi wa Hezbollah wameuwawa. Raia 24 wa Israel na wanajeshi 18 wa Israel pia wameshauawa.
Zaidi ya hayo, takriban Walebanon 100,000 na Waisraeli 60,000 wamelazimika kuondoka makwao na kumekuwa na uharibifu mkubwa wa mali kwa pande zote mbili. Hata hivyo Israel na Hezbollah hadi sasa hawajaingia katika vita kamili. Israel inawekeza nguvu zake nyingi dhidi ya Hamas huko Gaza, na Hezbollah inaonekana kuhofia mashambulizi kamili ya Israeli ambayo yataisumbua Lebanon yote.
Hezbollah ina zaidi ya roketi 150,000 na makombora ambayo yanaweza kuipiga Israeli yote. Israel imesema itailenga Lebanon yote kama vita vitatokea. Vita kamili itagharimu pande zote mbili za mgogoro.
Ongezeko kubwa la mivutano baina ya Israel na Hezbollah linatokea wakati kukiwa na ripoti kwamba Israel na Hamas zinakaribia muafaka angalau kwa sehemu ya makubaliano ambayo yatakayo sababisha kuachiliwa kwa mateka wa Israel na kusitisha mapigano kwa muda wa wiki sita.