Akizungumza Alhamisi katika Mkutano wa Muungano huo wa NASA uliofanyika katika bustani za Uhuru Park, mjini Nairobi, Odinga amesema "tunataka kubadilisha Kenya ili kila mtu apate manufaa."
“Waanzilishi wa taifa letu walitaka tupigane na umaskini, magonjwa na ujinga,” amesema Odinga.
Amesisitiza kuwa vijana wa Kenya ni lazima wapate fursa za ajira, wakina mama waweze kufanya kazi na bei za bidhaa zirudi chini.
Takribani miezi mitatu kabla ya uchaguzi mkuu kuandaliwa nchini Kenya, hatimaye Muungano wa Upinzani nchini humo NASA unaojulikana kama National Super Alliance unaowaleta pamoja viongozi wa vyama vingine tano umemtangaza mgombea wake.
Odinga aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo anapeperusha bendera ya chama chake katika kinyang’anyiro cha Urais na atamenyana na Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee katika uchaguzi mkuu wa Agosti nane mwaka huu.
Aidha, Kiongozi wa Wiper Democratic Movement Kalonzo Musyoka atakuwa Naibu wa Rais iwapo Muungano huo utatwaa madaraka kutoka kwa Kenyatta.
Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa kimekuwa kipindi kigumu kwa wafuasi wa upinzani nchini.
Amesema wengi wakielezea wazi kutamaushwa na kujikokota kwa Muungano huu kutaja kiongozi atakayepeperusha bendera ya Urais kukabana koo na Rais aliye madarakani Uhuru Kenyatta.
Lakini si wafuasi tu pekee; hata pamekuwapo na minong’ono miongoni mwa wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini kuwa huenda kitumbua kikaingia mchangani iwapo viongozi hawa wa upinzani hawatoweza kuzika tofauti zao na kumtangaza mgombea wa urais.
Muungano wa Nasa unawaleta pamoja viongozi wa tano kutoka vyama tofauti tofauti. Raila Odinga kutoka chama Orange Democratic Movement, Kalonzo Musyoka Wiper Democratic Movement, Musalia Mudavadi Amani National Congress, Moses Wetangula kutoka Ford Kenya na Isaac Ruto kutoka Chama cha Mashinani.
Kando na kumtangaza Bwana Odinga kupeperusha bendera ya Urais, Muungano huo umemtangaza Kalonzo Musyoka kuwa makamu wa Rais iwapo utatwaa madaraka. Katika mpangilio mwingine wa ugavi wa madaraka, Musalia Mudavadi atakuwa kiongozi mkuu wa baraza la mawaziri wadhifa ambao ni sawia na ule wa Waziri Mkuu kuendesha majukumu ya baraza. Bwana Mudavadi atakuwa na manaibu wake wawili watakaosimamia Wizara ya Ugatuzi na Mipango na Wizara ya Utumishi wa Umma; hawa wakiwa Isaac Ruto na Moses Wetangula katika usanjari huo.
Raila Odinga mwenye umri wa miaka 72 amewahi kugombea urais nchini kwa awamu tatu mwaka wa kenda mia tisini na saba, elfu mbili na sabakatika uchaguzi uliogubikwa na utata kati yake na Rais Mwai Kibaki na baadaye kupoteza kwa Rais aliye madarakani Uhuru Kenyatta miaka minne iliyopita.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennedy Wandera, Kenya