Ndege inayoaminika kuwa ya Ukraine imeishambulia Russia na kusababisha vifo

Jumba lililoharibiwa na shambulizi la ndege isiyokuwa na rubani, mjini Kyiv, Ukraine

Ndege isiyokuwa na rubani, inayoaminika kuwa ya Ukraine imepaa kilomita kadhaa ndani ya anga ya Russia na kusababisha mlipuko mbaya katika uwanja muhimu wa Russia unaotumika kutekeleza mashambulizi.

Wanajeshi wa Russia wamesema kwamba walitungua ndege hiyo na kuanguka kwenye uwanja wa jeshi wa Engels, ambapo wanajeshi watatu wameuawa.

Utawala wa Ukraine haujatoa ripoti yoyote, kwa kuzingatia sera yake ya kutozungumzia mambo yanayoendelea ndani ya Russia.

Uwanja huo wa kijeshi ni muhimu kwa kutekeleza mashambulizi ya mabomu ndani ya Kyiv na Ukraine imesema kwamba ndio umekuwa ukitumika katika siku za hivi karibuni kutekeleza mashambulizi dhidi ya mifumo muhimu.

Ndege hizo zimeundwa kutekeleza mashambulizi ya makombora ya nyuklia kama sehemu ya mpango wa muda mrefu wa kuzuia mashambulizi ya Russia.

Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema katika taarifa kwamba hakuna ndege iliyoharibiwa, lakini kurasa za mitandao ya kijamii za Russia na Ukraine zimesema kwamba ndege kadhaa zimeharibiwa.

Wanajeshi wa Russia wameondoka sehemu kadhaa

Vita vya Ukraine vinaingia mwezi wa 11.

Wanajeshi wa Ukraine wamelazimisha wanajeshi wa Russia kuondoa sehemu za kaskazini mwa Russia, baada ya kuwashinda nguvu.

Wanajeshi wa Russia wamelazimika pia kuondoka baadhi ya sehemu za mashariki na kusini, japo bado wanadhibithi sehemu za mashariki na sehemu kubwa ya kusini ambazo Putin amedai amenyakua kimabavu.

Maelfu ya raia wa Ukraine wamefariki katika vita hivyo na miji kadhaa kuharibiwa.

Maelfu ya wanajeshi kutoka pande zote mbili wameuawa.

Putin ametuma maelfu ya wanajeshi wa akiba, ikiwa ni hatua ya kwanza Russia kuwahi kuchukua tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia.

Mashambulizi ya kuharibu mfumo wa umeme ni 'uhalifu wa kivita'

Jeshi la Ukraine limesema mapema Jumatatu kwamba wanajeshi wa Moscow wametekeleza mashambulizi katika miji kadhaa katika majimbo ya Luhansk, Donetsk, Kharkiv, Kherson na Zaporizhzia.

Russia imekuwa ikilenga mfumo wa nishati wa Ukraine na kusababisha uharibifu mkubwa kwa makombora yanayotekelezwa na ndege zisizokuwa na rubani.

Moscow imesema kwamba lengo kubwa la kutekeleza mashambulizi hayo ni kuivunja moyo Ukraine kuendelea kupigana.

Ukraine imesema kwamba mashambulizi hayo hayana lengo lolote la kijeshi na yanalenga kuumiza raia wakati huu wa kipindi cha baridi kali. Ukraine imesisitiza kwamba inachofanya Russia ni uhalifu wa kivita.