Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, limesema wapiganaji wa Tigray wamewauwa dazani za raia katika kile kinachoonekana ni uhalifu wa vita kwenye miji miwili waliyokuwa wakiidhibiti katika jimbo la Amhara nchini Ethiopia. Mauaji yametokea kati ya Augusti 31 na septemba 9 mwaka huu, imesema ripoti mpya.
Mashahidi waeleza kwa wachunguzi wa HRW kwamba waliona wapiganaji wa Tigray katika vijiji vya Chema na Kobo wakiwauwa raia 49 kwenye matukio tofauti. Mkurugenzi wa shirika hilo anayeshughulikia maswala ya mizozo na mgogoro Lama Fakih amesema wapiganaji wa Tigray walifanya ukatili na kutojali maisha ya binadamu na sheria za vita kwa kuwauwa watu waliokuwa chini ya ulinzi wao.
Hata hivyo wapiganaji wa Tigray hawajajibu shutuma hizo. Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limetoa wito kwa umoja wa mataifa kufanya uchunguzi wa uhalifu wa vita na unyanyasaji uliofanywa na pande zote katika mzozo wa Tigray.
Hivi karibuni wanajeshi wa serikali walidai kukomboa tena miji katika majimbo ya Afar na Amhara iliyokuwa inashikiliwa hapo awali na wapiganaji wa Tigray. Mzozo wa Ethiopia uliochukua mwaka mzima umesababisha hali mbaya ya kibinadamu huku maelfu ya watu wakiuwawa na takriban watu milioni nane wanauhitaji mkubwa wa chakula .