Mwili wa Lemekani Nyirenda, ambaye alikuwa anasomea uhandisi kuhusu nyuklia, nchini Russia kabla ya kujiunga na jeshi, umefikishwa nyumbani na kupokelewa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kenneth Kaunda, mjini Lusaka, jana Jumapili.
Japo alikuwa mwanafunzi ambaye alikwenda Russia kwa ufadhili wa elimu ya juu, Lemekani alihukumiwa kifungo cha miaka 9 jela kwa makosa ya ulanguzi wa dawa za kulevya mnamo Aprili mwaka 2020.
Alisamehemewa baadaye kupitia mpango maalum wa serikali wa kutoa msamaha kwa masharti kwamba angekubali kushiriki katika vita nchini Ukraine, na aliuwawa akiwa katika mapigano.
Waziri wa mambo ya nje wa Zambia Stanley Kakubo amesema kwamba serikali ya Zambia imeiomba Russia kutoa maelezo zaidi kuhusiana na kifo cha Lemekani.