Mwendesha mashtaka wa Uturuki aomba kesi ya mauaji ya Jamal Khashoggi ihamishiwe Saudi Arabia.

Mwandishi wa Uturuki Hatice Cengiz, mchumba wa Jamal Khashoggi akisimama karibu na picha ya Khashoggi, katika hafla ya kumbukumbuku ya miaka mitatu ya mauaji yake, mjini Washington, Oktoba 1, 2021. Picha ya AFP.

Mwendesha mashtaka wa Uturuki katika kesi dhidi ya raia 26 wa Saudi Arabia walioshtakiwa kwa mauaji ya mwandishi wa gazeti la Washington Post Jamal Khashoggi, Alhamisi amewasilisha ombi la kushangaza akitaka kesi yao bila washukiwa kuwepo mahakamani, isitishwe na ihamishiwe Saudi Arabia.

Jopo la majaji halikutoa uamuzi kwa ombi la mwendesha mashtaka lakini wamesema barua itatumwa kwa wizara ya sheria ya Uturuki kupata maoni yake kuhusu uwezekano wa kuhamisha kesi hiyo kwenye mahakama za Saudi Arabia, shirika la habari la Serikali Anadou, limeripoti.

Kesi imeahirishwa hadi tarehe 7 Aprili.

Haya yanajiri wakati Uturuki imekuwa ikijaribu kuboresha uhusiano wake na Saudi Arabia, ambao ulizorota sana kufuatia mauaji ya Khashoggi Oktoba 2018.

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Melvut Cavusoglu amesema katika mahojiano Alhamisi kwamba maafisa wa Saudia wanashirikiana zaidi na Uturuki katika masuala ya mahakama, lakini hakufafanua.