Mwanasheria mkuu wa Kenya Githu Muigai ajiuzulu

Aliyekuwa mwansheria mkuu Githu Muigai.

Mwanasheria mkuu wa Kenya, Githu Muigai, alijiuzulu siku ya Jumanne. Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta, kupitia ujumbe wa Twitter, alisema  ameshangazwa na hatua hiyo, lakini akamshukuru kwa huduma yake ya miaka sita na nusu kama mshauri mkuu wa sheria wa serikali.

Na akizungumza muda mfupi baadaye kutoka ikulu ya Nairobi, Kenyatta alisema kwamba amemteua jaji Paul Kihara Kariuki, kama mwanasheria mkuu mpya.

Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa kuhusu sababu ya kujiuzulu kwa Muigai.

Kujiuzulu kwake kumejiri huku serikali ikilaumiwa vikali kwa kukosa kutii amri za mahakama hususan kufuatia mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini humo.

Alifahamika sana wakati wa kesi zilizowakumba rais Uhuru Kenyatta na naibu wake, William Ruto kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC, mjini The Hague, Uholanzi, ambapo aliwatetea kwa dhati viongozi hao.

Muigai aliteuliwa kama mwanasheria mkuu na rais Kenyatta kufuatia uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2013, na kuchukua nafasi iliyokuwa imeshikiliwa kwa muda mrefu na Amos Wako.

Kabla ya kuwa mwanasheria mkuu, Muigai alifanya kazi kama mjumbe maalum wa umoja wa mataifa kuhusu ubaguzi wa rangi na unyanyasaji.