Barr amesema kwamba wizara hiyo haijapata sababu yoyote inayoweza kubadlisa matokeo ya uchaguzi huo.
Mwanasheria mkuu ameliambia shirika la habari la Associated press kwamba waendesha mashtaka wa Marekani wamekuwa wakishirikiana na maafisa wa FBI kufuatilia madai yaliyokuwa yametolewa kuhusu uchaguzi huo lakini hakuna ushahidi wowote umepatikana.
Haya yanajiri wakati rais Donald Trump anaendelea kutoa madai kwamba kulifanyika wizi wa kura, na kukataa kukubali kwamba alishindwa na rais mteule Joe Biden.
Barr ni mmoja wa washirika wa karibu sana war ais Donald Trump na aliagiza wanasheria wa serikali kote nchini kuchunguza madai ya wizi wa kura iwapo ulifanyika.
Hali ni ngumu lakini msaada upo njiani unakuja – Biden
Wakati huo huo rais mteule wa Marekani Joe Biden ameahidi kuujenga uchumi wa Marekani unaowanufaisha Wamarekani wote, wakati atakapoingia madarakani Januari 20.
Uchumi wa Marekani unakabiliwa na tisho la janga la virusi vya Corona.
Biden amesema kwamba anajua kwamba hali ni ngumu sasa lakini anataka kila Mmarekani kujua kwamba msaada upo njiani unakuja.
Amesema hayo wakati akitangaza washauri wa ngazi ya juu wa uchumi akiwemo aliyekuwa mwenyekiti wa benki kuu Janet Yellen ambaye ameteuliwa kuwa waziri wa fedha.
Biden ametoa wito kwa senate kupitisha mswada wa kufadhili wafanyakazi na biashara mwezi huu wa Desemba kabla ya maseneta wapya waliochaguliwa kuanza mhula wao Januari.
Ameahidi kuwasilisha mapendekezo ya msaada wa kifedha kwa wamarekani punde tu atakapoingia madarakani.
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC