Mamia ya watu nchini Uganda walikusanyika kwenye ukumbi karibu na kijiji cha Bukwo, Uganda ili kuhudhuria mazishi hayo. Mauaji ya Cheptegei yalifanyika baada ya kurejea kutoka kwenye michezo ya Olimpiki mjini Paris, ambako alishiriki mbio za marathon Agosti 11 na kushika nafasi ya 44.
Wiki tatu baada ya kumalizika kwa Olimpiki, mpenzi wake wa zamani Dickson Ndiema Marangach, alidaiwa kumshambulia, wakati alipokuwa akitoka kanisani akiwa na watoto wake wawili wa kike, kwenye kijiji cha Kinyoro magharibi mwa Kenya, kulingana na ripoti za polisi.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, baba ya Cheptegei amesema kuwa binti yake aliwasilisha ripoti za malalamishi dhidi ya Marangach kwa polisi takriban mara tatu, ya mwisho ikiwa Agosti 30, siku mbili kabla ya kudaiwa kuuwawa naye.
Cheptegei alizaliwa Uganda 1991, na kisha baadaye akakutana na Marangach kwenye mazoezi nchini Kenya, ambako alihamia na kuendeleza ndoto yake ya kuwa mwanariadha ya kimataifa. Marangach pia aliripotiwa kufa siku chache baada ya Cheptegei, kutokana na majeraha ya moto aliyopata wakati wa shambulizi hilo.