Mahakama moja ya Uhispania, imeruhusu kufanyika kwa uchunguzi wa maiti ya aliyekuwa rais wa Angola Jose Eduardo dos Santos, aliyeaga dunia akiwa mjini Barcelona Ijumaa, wiki jana.
Binti yake, Tchize dos Santos, aliomba uchunguzi wa maiti yake ufanyika kwa sababu anaamini kulikuwa na mazingira ya kutiliwa shaka kuhusiana na kifo chake. Alisema mahasimu wake wa kisiasa hawakutaka aunge mkono upinzani, katika uchaguzi ujao wa Angola, BBC iliripoti.
Hali kadhalika, shirika hilo la habari liliripoti kwamba mwanasiasa huyo alitaka kuzikwa kwa faragha nchini Uhispania, lakini serikali ya Angola inafanya mipango, ikitaka mwili wake urejeshwe nchini mwake kwa mazishi rasmi ya kiserikali.
Mzwanasaiasa huyo mkongwe, aliyekuwa na umri wa miaka 79 alifariki katika zahanati ya Teknon mjini Barcelona, ambako alikuwa akipokea matibabu, na alikuwa ameugua kwa muda mrefu, kulingana na taarifa ya afisi ya rais.