Chama tawala nchini Uganda Jumatano kilimuidhinisha rais Yoweri Museveni kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2021.
Uamuzi huo wa Chama cha National Resistance Movement – NRM – umekuja baada ya bunge kupitisha muswada mwaka 2017 ulioondoa kikomo cha umri wa urais kuwa miaka 75, uamuzi ambao umefunguliwa shauri katika mahakama ya kikatiba ya Uganda.
Ni mara ya pili kwa bunge lenye wawakilishi wengi wa chama cha NRM kubadilisha katiba ya Uganda kumruhusu rais Yoweri Museveni kuongeza muda wake wa kukaa katika mamlaka baada ya kuondoa ukomo wa muhula wa urais mwaka 2005.
Museveni amekuwa madarakani toka mwaka 1986 baada ya kuwa kiongozi wa waasi, na kwa kipindi chote utawala wake umekuwa ukishutumiwa kwa rushwa, uvunjifu wa haki za binadamu na huduma mbaya za kijamii.
Kwa sasa Museveni ana umri wa miaka 74.