Museveni: DRC imeruhusu jeshi la Uganda kushambulia ngome zaidi za waasi

Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kwamba serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imewaruhusu wanajeshi wa Uganda UPDF, kuingia sehemu zaidi ambazo waasi wa kundi la Allied Democratic Forces ADF wanaaminika kujificha, na kuwashambulia waasi hao.

Katika ujumbe wa Twitter, Museveni amesema kwamba jeshi la Uganda limeruhusiwa kutekeleza mashambulizi nje ya Kivu Kaskazini, na kuua mamia ya waasi wa ADF.

“Ijumaa Novemba 4, 2022, kwa ruhusa ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wanajeshi wa Uganda walishambulia kambi kubwa ya ADF,” ameandika Museveni akiongezea kwamba “adui sasa amekimbia na kuondoka nje ya mipaka yetu tunayoruhusiwa kumshambulia. Magaidi wapumbavu hawajui kwamba tunaweza kuwafikia katika muda wa dakika chache sana na wala sio masaa na kuwashambulia kwa moto mkali sana hata nje ya sehemu tunayoruhusiwa kufanya kazi.”

Museveni amebandika video ya shambulizi la jeshi la Uganda, kwenye ujumbe wake wa Twitter.

Ni nadra sana kwa Museveni kuandika operesheni za kijeshi kwenye mitandao ya kijamii.

“Wamepata zawadi ambayo huwa wanatafuta. Popote waendapo, tutawafikia, serikali ya DRC itakapoturuhusu,” ameandika Museveni akiongezea kwamba "naandika haya kwenye Twitter kwa sababu ni muhimu kwa Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla kujua kwamba tuna uwezo wa kusuluhisha matatizo yetu ya usalama wenyewe."