Museveni atoa tahadhari ya Ebola

Kirusi cha Ebola ambacho kimeingia Uganda kwa mara nyingine

Wagonjwa wawili wameripotiwa Kampala, mmoja afariki katika hospitali ya Mulago

Rais wa Uganda ametahadharisha wananchi wa Uganda dhidi kugusana gusana baada ya muathirika wa kirusi kikali cha homa ya Ebola kuripotiwa katika mji mkuu Kampala.

"Wizara ya afya inawasiliana na watu wote waliokutana na mgonjwa huyo," alisema Rais Museveni katika hotuba ya taifa akiongeza kuwa watu 14 wamefariki tangu homa ya Ebola kulipuka magharibi mwa nchi wiki tatu zilizopita.

Wagonjwa wawili wameripotiwa Kampala, mmoja akafariki katika hospitali kubwa ya Mulago. Rais ametaka watu wasishikane mikono wanaposalimiana kuepuka kueneza ugonjwa huo.

Madakati saba na wafanyakazi wengine wa afya 13 katika hospitali ya Mulago wapo katika karantini baada ya wagonjwa "mmoja au wawili" kupelekwa katika hospitali hiyo.