Nitakabiliana na utovu wa usalama Uganda - Museveni

Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Rais wa Uganda Yoweri Museveni, alilihutubia bunge la nchi hiyo Jumatano na kueleza kile alichokiita "mikakati ya kukabiliana na utovu wa usalama."

Katika hotuba yake, Museveni alionya kwamba hakuna yeyote anayeweza kuiyumbisha nchi hiyo kwa kutumia silaha.

Aidha, alisema kuna changamoto za usalama wa nchi kwa sababu bajeti ya ulinzi ni dogo mno.

Hata hivyo, rais huyo alitetea utawala wake na kudai kuwa hii ndiyo mara ya kwanza kwa kipindi cha miaka 500, ambapo Uganda ina usalama kutoka kona moja hadi nyingine.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni akilihutubia bunge. Juni 20, 2018.

Museveni aliwakosoa maafisa wa polisi kwa jinsi walivyolishughulikia suala la mauaji yaliyotekelezwa mjini Entebbe na kuamrisha kwamba bunduki zote zifanyiwe ukaguzi wa alama za vidole ili kubaini ni nani anazitumia.

"Hii inamaanisha bunduki zote zisizo halali zitatambuliwa,” alisema.

Kadhalika rais huyo alisema kuwa serikali yake ina mipango ya kuweka kamera kwenya barabara za mijini na kwamba kuna haja ya alama za viganja vya mkononi kuwa kwenye vitambulisho kama njia moja ya kukabiliana na utovu wa usalama.

Kiongozi huyo pia alipendekeza kwa mara nyingine tena kwamba kila Mganda achukuliwe chembchembe za DNA zitakazohifadhiwa kwenye kompyuta katika juhudi za kuimarisha hali ya usalama.

"Mimi siogopi kuchukuliwa chambachembe za damu. Wahalifu ndio wanaogopa," alisema Museveni.

Utawala wa Museveni umeendelea kukosolewa kwa hali inayozorota ya usalama nchini, huku baadhi wakisema serikali yake haichukui hatua za kutosha kukabiliana na hali hiyo.

Kwa mujibu wa gazeti la Monitor, hotuba yake ya Jumatano ilihudhuriwa tu na wabunge 285 kati ya 458.