Mugabe ajitokeza hadharani

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe alionekana hadharani kwa mara ya kwanza Ijumaa, tangu jeshi la nchi hiyo kumzuilia nyumbani kwake siku ya Jumatano.

Kiongozi huyo mkongwe, akiwa amejivika kofia, mavazi ya rangi ya samawati na majano, alihudhuria sherehe ya kuhitimu katika chuo kikuu, kilicho kwenye mji mjuu, Harare, huku akishangiliwa na umati wa watu.

Wazimbabwe wanatumai kwamba mzozo wa kisiasa unaoikabili nchi hiyo utatatuliwa kwa haraka, huku viongozi wa upinzani, dini na wanaharakati wakimtaka Mugabe kung’atuka madarakani baada ya jeshi kuchukua udhibiti wa serikali.

Hata hivyo, ripoti zilieleza kwamba Mugabe hajasalimu amri. Wakati huo huo, rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma aliliambia bunge la nchi yake kwamba ni mapema mno kuchukua msimamo wowote kuhusiana na mzozo huo wa Zimbabwe.

Donald Yamamoto, Kaimu waziri wa mambo ya nje wa Marekani kuhusu masuala ya Afrika, alisema kuwa Marekani inatumai kwamba Zimbabwe inaingia kwenye awamu mpya ya uongozi.