Mtuhumiwa wa ugaidi Kenya apewa dhamana

  • Josephat Kioko

Imam Sheikh Aboud Rogo Mohammed kwenye baraza ya mahakama moja mjini Mombasa

Sheikh Aboud Rogo Mohammed mtuhumiwa wa ugaidi huko Kenya apewa dhamana.

Mtu anayetuhumiwa kwa ugaidi nchini Kenya amepewa dhamana na mahakama moja ya Mombasa alikokuwa amezuiliwa kwa wiki tatu.

Mtuhumiwa huyo Sheikh Aboud Rogo Mohamed hata hivyo atalazimika kutoa dhamana ya dola 50,000 ili kutoka jela.

Kiwango hiki ni miongoni mwa dhamana za juu zaidi kuwahi kutozwa mshtakiwa katika kesi ya kosa la jinai nchini Kenya.

Hakimu Mwandamizi wa Mombasa, Karemi Mwangi ameuagiza mhubiri huyo wa kiislamu kuwasilisha wadhamini watatu wa kiasi sawa cha dhamana aliyopewa.

Sheikh Rogo amezuiliwa tangu Januari 29 mwaka huu, alipokamatwa katika kijiji cha Kanamai jimbo la Kilifi, takriban kilometa 40 kaskazini mwa Mombasa.

Polisi maalum wa Kenya wa kupambana na ugaidi walisema Sheikh Rogo alikuwa anamiliki silaha hatari nyumbani kwake, ikiwemo bunduki aina ya AK-47, bastola mbili, risasi 113, gruneti mbili za mkono na milipuko 112.

Sheikh Rogo alifunguliwa mashtaka sita ikiwa ni pamoja na kujiandaa kutenda uhalifu, kumiliki silaha na milipuko bila kibali.

Hata hivyo familia yake pamojana mawakili wanaomtetea wamesema kuwa maafisa wa polisi walipanga njama za kumuwekea silaha hizo.

Umamuzi wa mahakama kumuachia Imam huyo kwa dhamana unafuatia mjadala mkali mahakamani, baina ya wakili wake Mbugua Mureithi na kiongozi wa mashtaka Alex Wasike.

Waendesha mashtaka kwa niaba ya idara ya upelelezi Kenya wanamtaja Imam huyo wa msikiti kama mtu hatari, ambaye anaweza kuvuruga ushahidi katika hiyo inayohusu ugaidi.

Kulikuwa na ulinzi mkali ndani na nje ya mahakama ya Mombasa wakati hakimu Karemi Mwangi alipotoa uamuzi wake.

Hii ni kesi ya tatu dhidi ya Imam huyo wa msikiti, katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Mwaka 2002 alihusishwa na mauaji ya watu 15 kufatia shambulizila kigaidi katika hoteli ya kitalii eneo la Kikambala kwenye pwani ya Kenya, hoteli iliyokuwa inamilikiwa na mwekezaji kutoka Israel.

Alifutiwa mashtaka hayo mwaka 2005 baada ya kukosekana ushahidi wa kutosha. Sheikh Rogo alishtakiwa tena mwishoni mwa 2010 kufuatia shambulizi dhidi ya basi la abiria katika mji wa Nairobi, ambalo lilikuwa linaelekea Kampala, Uganda.