Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa imesema tayari imeshaanza uchunguzi kufuatia taarifa hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jumatano Naibu Waziri katika wizara hiyo Dkt Suzan Kolimba amethibitisha kuwepo kwa tatizo hilo ambalo inadaiwa raia hao wa Tanzania wanaondolewa kwenye maeneo waliyokuwa wanaishi na kufanya biashara.
Amesema ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji unaendelea kufanya mazungumzo ya kidiplomasia na serikali ya nchi hiyo ili kujua sababu zilizopelekea watanzania waliokuwa wakiishi kihalali.
Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa kumekuwa na madai mengine kwamba mali zao zimeharibiwa pamoja na kunyang'anywa pasi zao za kusafiria.
Hata hivyo wizara imetoa tamko kuwa Tanzania imeendelea kuwa mahusiano mema na nchi ya msumbiji na hivi karibuni tu imekuwa na mkutano wa pamoja juu ya masuala kadhaa yanayohusu kuboresha ushirikianokati ya nchi hizo.
Madai ya kufukuzwa na kunyanyaswa raia wa Tanzania waliopo Msumbiji yaliyoanza kusambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii hapa nchini tangu Jumanne.
Kumekuwa na hisia tofauti kati ya watanzania walio wengi kutokana na historia ya nchi hizi mbili tokea wakati wa ukombozi wa msumbiji chini ya baba wa taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Eduardo Mondlane na baadaye hayati Samora Machel.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Dina Chahali, Tanzania