Msichana aliyekimbia Saudi Arabia hatolazimishwa kurudi kwao

Rahaf Mohammed Alqunun akiwa uwanja wa ndege huko Bangkok, 7 Januari 2019

Rahaf Mohammed Alqunun mwenye miaka 18 raia wa Saudi Arabia hivi sasa yupo chini ya huduma za UNHCR na awali alizuiliwa Thailand wakati akijaribu kukimbilia Australia

Maafisa wa Thailand walisema msichana raia wa Saudi Arabia ambaye alizuiliwa huko Thailand akiwa anajaribu kukimbilia Australia kutafuta hifadhi ameondoka uwanja wa ndege wa Bangkok na yupo chini ya huduma za idara ya wakimbizi ya Umoja wa Mataifa.

Mkuu wa polisi cha kitengo cha uhamiaji Thailand Meja Jenerali Surachate Hakparn aliwaambia waandishi wa habari kuhusu kesi ya Rahaf Mohammed Alqunun kwamba yupo chini ya huduma za UNHCR hivi sasa lakini pia walipeleka mlinzi wa Thailand kumsaidia binti huyo. Hakparn alisema Rahaf hatolazimishwa kurudi Saudi Arabia.

Rahaf Mohammed Alqunun

Msichana huyo wa miaka 18 alikimbia Kuwait wakati wa likizo ya kifamilia na aliwasili kwenye uwanja wa ndege wa Suvarnabhumi Jumamosi usiku. Alijifungia ndani ya chumba cha hoteli kwenye uwanja wa ndege na siku ya Jumatatu alituma ujumbe kadhaa kwenye mtandao wa Twitter akiomba aruhusiwe kukutana na mtu yeyote kutoka Umoja wa Mataifa.

Katika video ya awali Rahaf alionekana akitembea ndani ya chumba cha hoteli huku akisema “anataka kuishi”.