Msafara wa wahamiaji wasonga mbele kwenda Marekani

Msafara wa mamia ya wahamiaji uliondoka katika mji wa kusini mwa Mexico, Tapachula, Jumapili, kuelekea mpaka wa kusini wa Marekani.

Msafara mdogo unapanga kujiunga na ule mkubwa zaidi ulioondoka siku sita zilizopita na kwa sasa umesimamishwa takriban kilomita 40 kaskazini mwa mji wa Huixtla.

Waandaaji wamesema msaafara wa kwanza ulifurika na kufikia watu 7,000 huku serikali katika jimbo la Chiapas kusini ikisema inakadiria kundi hilo kuwa watu 3,500.

Wahamiaji wengi wanakimbia umaskini na ukosefu wa utulivu wa kisiasa katika nchi zao, kutoka Cuba, El Salvador, Guatemala, Haiti, na hasa Honduras na Venezuela, kulingana na shahidi wa shirika la habari la Reuters.

Rais wa Marekani, Joe Biden, anaegombania mhula wake wa pili anapata msukumo mkubwa wa kupunguza idadi ya watu wanaovuka mpaka kimagendo kuingia Marekani, kutokea Mexico.