Malaysia yatuma msaada wa dharura Somalia

Mzoga wa wanyama wanaokufa kwa sababu ya ukame ukipigwa picha

Malaysia inatuma vikosi vyake Somalia ikiwa ni sehemu ya msaada wa dharura kuisaidia Somalia katika janga la ukame na kuweza kuwaokoa maelfu ya watu, maafisa wa serikali ya Somalia na wanadiplomasia wamesema Jumamosi.

“Naweza kuthibitisha ripoti hizo, na maelezo zaidi yatatolewa wakati ujumbe wa Somalia ukiongozwa na Naibu Waziri Mkuu, Mohamed Omar Arte, unaozuru Malaysia hivi sasa, utaporejea nchini, Waziri wa Habari wa Somalia Mohamed Abdi Baryir ameiambia VOA.

Akizungumza na waandishi wa habari Kuala Lumpur, Waziri wa Ulinzi Datuk Seri Hishammuddin amesema nchi yake itapeleka maafisa watatu na wafanyakazi 17 kutoka katika kitengo Muhimu cha Tiba cha Jeshi lake nchini Somalia.

Kikosi cha ardhini, kitachokuwa na afisa mmoja na wafanyakazi 10, watatoa ulinzi kwa ujumbe utakaotumwa Somalia. Shehena ya chakula na madawa vitasafirishwa kwa ndege aina ya Hercules C-130 kwenda Somalia, waziri amesema.

Waziri pia amesema kuwa vikosi, pamoja na vifaa, vitakusanywa kutoka Riyadh, Saudi Arabia, ambako Malaysia ilikuwa imetuma idadi ndogo ya vikosi vyake kusaidia kuwaondoa wananchi wa Malaysia huko Yemen.

Lakini, wengi wanaamini kuwa vikosi vya Malaysia ni sehemu ya ushirika wa kijeshi wa Riyadh katika kupambana na wapiganaji wa Houthi huko Yemen.

Mwanadiplomasia wa Somalia katika ujumbe huo ambaye ametaka jina lake lisitajwe kwa sababu yeye sio mzungumzaji rasmi kuhusu suala hilo amesema uamuzi huo umefikiwa Jumanne kufuatia mkutano kati ya Naibu Waziri Mkuu Mohamed Omer Arteh na maafisa wa ngazi ya juu wa Malaysia, akiwemo waziri wa ulinzi.

“Wakati wa mkutano huo, wajumbe wa Somalia waliiomba Malaysia iwape msaada na pia ulinzi katika barabara mbalimbali zinazopitika nchini Somalia, na Malaysia imekubali mara moja kuwasaidia,” Mwanadiplomasia huyo amesema. “Malaysia itazungumza na washirika wake Uarabuni na Asia juu ya kuisaidia Somalia.