Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May ameeleza kuwa inaelekea tukio hili ni kitendo cha ugaidi. Mlipuko huo ulitokea katika ukumbi wa tamasha la muziki.
Iwapo uchunguzi utathibitisha kuwa ni shambulio la kigaidi, litakuwa ni tukio baya zaidi kuliko yote yaliyowahi kutokea katika kumbukumbu ya Uingereza tangu Julai mwaka 2005.
Katika tukio hilo la mwaka 2005 zaidi ya watu 50 walikufa kwenye mtiririko wa mabomu mjini London.
Mashuhuda wa mlipuko huo wa Manchester wamesema mwanamuziki wa Marekani Ariana Grande alikuwa amemaliza kuwatumbuiza mashabiki wake, wakati ghafla mlipuko mkubwa ulisikika na uliotikisa eneo lote.
Athari za bomu hilo lilionekana kutokana na misumari iliyokuwa imeenea sakafuni na harufu ya moshi uliotokana na mabomu hayo.
Hivi sasa eneo ambalo mlipuko ulitokea limezingirwa na polisi wametandaa na wanaendelea kushika doria katika eneo lote la tukio hilo.
Vyanzo vya habari nchini Uingereza vimesema kuwa Waziri Mkuu Theresa May anatarajiwa kuongoza kikao cha dharura cha kamati ya usalama baadaye leo.
Pia vimesema kuwa habari ambazo bado hazijathitishwa kutoka kwa maafisa wa Marekani ambao hawakutajawa, zinasema kuwa shambulizi hilo lilifanywa na mshambuliaji wa kujitoa mhanga.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Uingereza Ukumbi wa Manchester ambao ulikuwa ukifahamika awali kama ukumbi wa wanaume, ndio ukumbi mkubwa zaidi mjini humo wenye uwezo wa kuwachukua watu 18,000
Barabara ya ukumbi huo inuangana na kituo cha treni cha Victoria kati kati mwa mji.
Ukumbi huo hutumiwa kuandaa tamasha za manyota wakuu kama Ariana Grande nyota wa runinga mwenye umri wa miaka 23 ambaye sasa ni nyota wa muziki wa pop.