Mkosoaji mkubwa wa serikali ya Burundi ameikosoa serikali ya Marekani kwa kuondoa vikwazo dhidi ya nchi yake akisema hakuna kilichobadilika, kuhalalisha hatua hiyo.
Katika mahojiano na shirika la habari la AFP, Alexis Sinduhije kiongozi wa chama cha upinzani cha Movement for Solidarity and Democracy (MSD) alisema kwamba inashangaza kuwa nchi yenye nguvu kama hiyo inaweza kuliangalia suala la Burundi kwa macho mepesi sana. Akiongeza kuwa raia wa Burundi wanakufa kila siku, ripoti za haki za binadamu zinazungumza juu yake, waangalizi walioko nyumbani wanalijua hilo.
Washington wiki iliyopita, iliondoa vikwazo vilivyowekwa miaka sita iliyopita, ikisifu uchaguzi, kushuka kwa ghasia na mageuzi yaliyofanywa na Rais Evariste Ndayishimiye.
Mwandishi huyo wa habari wa zamani ambaye kwa sasa anaishi Ubelgiji ni mmoja wa wapinzani wakubwa wa nchi hiyo na kwa muda mrefu amekuwa mtu mwenye mtazamo tofauti.