Mpinzani wa Saudia auawa Lebanon

Mwanamfalme wa Saudia Mohammed Bin Salman, akikutana na waziri mkuu wa Lebanon Saad Hariri mjini Riyadh, October 30, 2017. Picha ya AP

Mpinzani wa kisiasa wa Saudia Menea Al-Yami aliuawa nchini Lebanon, chama cha upinzani cha Saudia National Assembly Party (NAAS) na chanzo cha usalama cha Lebanon wamesema Jumapili.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye Twitter, NAAS, chama cha upinzani kilichoanzishwa na raia wa Saudia wengi wao wakiishi uhamishoni, kimesema Yami aliuawa katika mazingira ya kutatanisha, siku ya Jumamosi.

Kimeomba uchunguzi huru na wa wazi kuhusu mauaji hayo, na kusema kwamba viongozi wa Saudia watawajibishwa kwa kushindwa kulinda usalama wa raia wanaotafuta uhuru zaidi nje ya nchi.

Maafisa wa usalama wa ndani nchini Lebanon wamesema raia huyo wa Saudia mwenye umri wa miaka 42 alichomwa kisu hadi kufa na ndugu zake wawili katika ugomvi wa kifamilia siku ya Jumamosi, bila pamoja na hivo kutangaza jina la muathiriwa.

Wamesema maafisa wa usalama wamewakamata ndugu hao wawili Jumapili na kwamba walikiri kuhusika na mauaji hayo.

Chanzo cha usalama cha Lebanon kimeithibitishia Reuters kwamba muathiriwa aliyechomwa kisu ni Menea al-Yami.

Balozi wa Saudia nchini Lebanon, Waleed al-Bukhari, amepongeza juhudi za maafisa wa Lebanon kufichukua ukweli na kuwafikisha wahusika mbele ya vyombo vya sheria katika ujumbe kwenye Twitter.

Yami, kutoka dhehebu dogo la Waislamu Washia wa Ismailia huko Saudia, amekuwa akiishi nchini Lebanon tangu mwaka wa 2015, amesema afisa mwandamizi wa chama cha NAAS Yahya Assiri. Alikuwa akijaribu kupata sehemu salama katika nchi ya tatu.

Yami alisaidia kuanzisha chama cha NAAS mwaka wa 2020. Kundi hilo lilitetea kuwepo bunge lililochaguliwa nchini Saudia, pamoja na misingi ya kikatiba ili kuhakikisha bunge, mahakama na serikali, mihimili hiyo mitatu inafanya kazi kwa uhuru bila kuingilia kazi ya mwingine.