Jaji wa Mahakama Kuu amesema katika uamuzi wake kuwa Diane Rwigara na mama yake, ambao walikamatwa pamoja mwaka 2017, wataachiwa huru mara moja lakini kwa sharti ya kuwa hawaruhusiwi kuondoka mjini Kigali “bila ya kibali.”
Wakati jaji akisoma hukumu hiyo katika chumba cha mahakama ambacho kilikuwa kimejaa wanadiplomasia, waandishi wa habari na ndugu wa wanawake hao waliokuwa wamevaa nguo za kifungoni rangi ya pinki, chumba cha mahakama ghafla kilijawa na furaha na watu kadhaa walipiga kelele “Mungu Asifiwe!”.
Rwigara na mama yake walihukumiwa kifungo Octoba 2017 kwa mashtaka ya uchochezi na kughushi ambayo yalionekana kuwa ni ushawishi wa kisiasa.
Mwanamke huyo mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 37 na mwanaharakati mara nyingi amemtuhumu Kagame kwa kuzuiya upinzani na kukosoa chama chake cha Rwanda Patriotic Front kwa kuendelea kushikilia madaraka tangu ilipoingia madarakani kupitia mtutu wa bunduki ikiwa ni hatua ya kumaliza mauaji ya halaiki mwaka 1994.
Uamuzi wa mahakama umekuja wiki kadhaa baada ya Rwanda kumuachia huru Victoire Ingabire, kiongozi wa upinzani ambaye alikuwa ametumikia miaka sita ya kifungo chake cha miaka 15, baada ya Kagame kutoa msamaha kwa kutumia nafasi yake ya urais.