Mpinzani Venezuela agoma kufika mahakamani

Mgombea wa upinzani wa Venezuela, Edmundo Gonzalez, ambaye anasisitiza kuwa yeye ndiye mshindi halali wa uchaguzi wa urais wa Julai 28, Jumatano alishindwa kutii mwito wa Mahakama ya Juu iliyoamuru afikishwe mahakamani kwa ajili ya ukaguzi wa uchaguzi uliopingwa wa Julai 28.

Tume ya taifa la uchaguzi inayoungwa mkono na serikali iliidhinisha matokea ya kumpa ushindi Rais Nicolas Maduro, na kumwezesha kutawala kwa muhula wa tatu wa miaka sita, uamuzi ambao ulikataliwa na upinzani na kusababisha maandamano makubwa.

Upinzani unaona pia Mahakama ya Juu ipo katika upande wa kushirikiana na serikali ya Maduro.

Marekani na nchi kadhaa za Amerika Kusini ni miongoni mwa mataifa ambayo yanamtambua Gonzalez kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais na wametoa mwito kwa maafisa wa uchaguzi wa Venezuela kuchapisha taarifa zao za uchaguzi.

Maafisa wa uchaguzi wanasema wamekabidhi hesabu zao kwa mahakama.