Mpango athibitishwa na bunge kuwa Makamu Rais wa Tanzania

Waziri wa Fedha Dkt Philip Mpango

Tukio hili limefanyika kwa mujibu wa katiba ya nchi baada ya kufariki aliyekuwa Rais wa Tanzania hayati John Pombe Magufuli hapo Machi 17, 2021 katika hospitali ya Mzena jijini Dar Es Salaam

Aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania, Dr. Philip Isdory Mpango amethibitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Makamu wa Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya jina lake kuwasilishwa Bungeni kwa mapendekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Kikao cha kamati Kuu ya CCM kimefanyika Jumanne jijini Dodoma ambapo kwa kushauriana na chama hicho ndipo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alipowasilisha jina la Dr Philip Mpango kama mteule wa nafasi ya Makamu wa Rais. Tukio hili limefanyika kwa mujibu wa katiba baada ya kufariki aliyekuwa Rais wa Tanzania hayati John Pombe Magufuli hapo Machi 17, 2021.

Wabunge katika bunge la Tanzania wamemthibitisha Mpango kuwa Makamu Rais wa nchi hiyo

Baada ya jina hilo kuwasilishwa kwa spika wa bunge Job Ndugai, Dr Mpango ambaye pia alikuwa Mbunge wa Buhigwe mkoani Kigoma alipigiwa kura na kuthibitishwa na Bunge kwa kupata kura zote za “NDIO” zilizopigwa ambazo ni 363.

Baadhi ya wabunge waliozungumza kabla ya jina la Dr. Mpango kupigiwa kura walisifu mapendekezo hayo ya Rais Samia Suluhu Hassan na kwamba Dr. Mpango ni mtu sahihi wa kumsaidia rais katika majukumu yake

Dr. Mpango anatarajiwa kuapishwa Jumatano jijini Dodoma na Jaji Mkuu wa Tanzania, kushika nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.