Kamishna London asema ni miujiza watu kuwa hai katika jengo la Grenfell

Mtu anasoma ujumbe wa maombolezi katika ukuta wa jengo lililoharibiwa na moto London.

Ofisi ya wazima moto London imesema Alhamisi wafanyakazi wake walifanikiwa kuuzima moto ambao tayari umeuwa watu 17 na idadi inatarajiwa kuongezeka.

Moto huo uligubika jengo hilo lenye ghorofa 24 siku moja iliyopita.

Kamanda wa polisi Stuart Cundy amesema kuwa watu 37 wanaendelea kupata matibabu hospitalini, huku 17 miongoni mwao wakiwa katika hali mbaya. Amaongeza kusema kuwa wanachofanya sasa ni kutambua na kutafuta waliokosekana.

“Ni msiba mkubwa, kwani sasa hatuna matarajio ya kumkuta mtu yoyote akiwa hai,” Kamishna wa Ofisi ya Zima Moto ya London Dany Cotton amekiambia kituo cha televisheni cha Sky News.

“Kutokana na moto mkali na joto kali inamaanisha itakuwa ni miujiza kwa mtu yoyote kukutikana akiwa hai.”

Moto huo ulitambaa haraka katika Jengo hilo refu la Grenfell huko London Magharibi wakati wa alfajiri Jumatano, ukiwazingira wakazi wa jumba hilo. Jengo hilo lilikuwa na wateja wanaokadiriwa 120 na watu waliokuwa wanaishi ndani ya jengo hilo ni 600.

Cotton amesema itachukuwa muda kwa wazima moto kufanya upekuzi ndani ya jengo na kugundua mtu yoyote aliachwa humo ndani. Pia alisema wakati wapelelezi wanatafuta kujua chanzo cha moto huo, bado ni mapemo mno kuweza kukisia ni nini kilikuwa chanzo cha moto huo.