Moto umezuka Alhamisi katika kiwanda cha betri za magari kinachomilikiwa na wizara ya ulinzi ya Iran, kwa mara ya pili katika chini ya wiki moja, vyombo vya habari vya serikali vimeripoti.
Hakuna mtu aliyejeruhiwa katika moto huo, ambao ulilipuka katika eneo ambalo taka za plastiki zimehifadhiwa, televisheni ya serikali imesema.
Vyombo vya habari vya Iran vilisambaza picha na video za safu ya moshi mweusi ukitanda angani kaskazini mwa mji mkuu, Tehran.
Jeshi la kawaida la Iran na walinzi wa kimapinduzi wanaendesha viwanda kadhaa nchini humo, ambavyo vingi vinazalisha bidhaa za kiraia.
Iran imeshuhudia mfululizo wa matukio ya moto na makosa mengine katika vituo vyake vya kijeshi kwa miaka mingi, na mara nyingi imekuwa ikimtuhumu adui yake mkuu taifa la Israel kwa hujuma.
Mwezi uliopita, Iran ilisema Israel ilijaribu kuhujumu mpango wake wa makombora ya mbali kwa kutumia vifaa vya kigeni vibovu vinavyoweza kulipuka.