Mnangagwa aliwasili nchini Zimbabwe mapema Jumatano kutoka nchini Afrika Kusini, ambako alikimbilia baada ya kuachishwa kazi na aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Robert Mugabe.
Mwanasiasa huyo aliwashukuru raia wa Zimbabwe kwa kudumisha amani wakati wa mzozo wa kisiasa uliomkabili Mugabe na kuongeza kwamba alitorokea Afrika Kusini baada ya kupata habari kwamba kulikuwa na njama za kumuua.
"Mtakumbuka pia kwa wakati mmoja walijaribu kuniua kwa kuniwekea sumu," alisema Mnangagwa.
Rais huyo wa zamani alijiuzulu Jumanne kufuatia shinikizo kutoka pembe mbali mbali. ZANU-PF ilimuondoa Mugabe kwenye uongozi wake na kumteua Mnangagwa kama kiongozi mpya.
Aidha chama hicho, kilicho na wajumbe 159 kwenye bunge la taifa, kilimfukuza mkewe Mugabe kutoka kwa chama hicho.
Grace Mugabe alikuwa kiongozi wa tawi la wanawake kwenye chama hicho na alishutumiwa kwamba alichochea kufutwa kazi kwa makamu huyo wa rais na kwamba alimshinikiza mumewe kumuachia madaraka kama rais wa Zimbabwe.
Kwenye hotuba yake ya Jumatano, Mnangagwa alisema atafanya hotuba rasmi baada ya kuapishwa kama rais mwendo wa saa nne asubuhui siku ya Ijumaa.