Rais wa Russia Vladimir Putin, Jumatatu alimpa uraia wa Russia Edward Snowden, mkandarasi wa zamani wa usalama wa Marekani, ambaye alifichua habari kuhusu nyaraka za siri za kina kuhusu mipango ya uchunguzi wa serikali na kisha kutoroka Marekani kukwepa kufunguliwa mashtaka.
Snowden, mwenye umri wa miaka 39, alikuwa mmoja wa wageni 75 waliopewa uraia na kiongozi huyo wa Russia lakini akasema hana nia ya kuukana uraia wake wa Marekani.
Russia ilimpa hifadhi mnamo mwaka wa 2013, na amekuwa akiishi humo tangu wakati huo.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani mara moja ilikejeli hali mpya ya uraia wa Snowden aliyoipata nchini Russia ikisema "huenda akaandikishwa" kupigania Russia katika uvamizi wake wa miezi saba sasa nchini Ukraine.
Lakini Putin alisema ni wale tu walio na uzoefu wa awali wa kijeshi ambao wataitwa, ingawa kumekuwa na ripoti nyingi kwamba wengine wameitwa pia, ikiwa ni pamoja na wanaume waliokamatwa kwenye maandamano ya kupinga hatua hiyo ya Putin.