Mlipuko wa kipindupindu kwenye kambi ya wakimbizi Cameroon

Wanajeshi wa Cameroon wapiga doria karibu na mpaka wa Nigeria. Machi 21, 2019

Mamlaka za Cameroon zimesema Jumatatu kwamba zinafanya kila juhudi kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu kwenye kambi ya wakimbizi lenye msongamano mkubwa karibu na mpaka wake wa kaskakazini na Nigeria.

Katika muda wa wiki moja iliyopita, watu watatu wamekufa kutokana na mlipuko huo kwenye kambi ya Manawao, huku wengine 19 wakiambukizwa bakteria zake ambazo husababishwa na chakula au maji machafu.

Mwanzoni kambi hiyo ilikuwa itoe hifadhi wa chini ya wakimbizi 15,000, lakini kwa sasa ina takriban wakimbizi 76,000 kutoka Nigeria waliokimbia mashambulizi kutoka kundi la kigaidi la Boko Haram.

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi UNHCR nchini Cameroon Helen Ngoh amesema kwamba wanahitaji msaada wa dharura ili kudhibiti hali pamoja na kuzuia milipuko mipya katika siku zijazo. UNHCR limesema kwamba linachunguza iwapo ugonjwa huo umeenea miongoni mwa wenyeji.