Mkuu wa Mkoa wa zamani Abbas Kandoro kuzikwa Iringa

Makamu wa Rais Samia Suluhu akimhani mke wa Mkuu wa Mkoa wa zamani marehemu Abbas Kandoro

Mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania wamejitokeza kuuaga mwili wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wa zamani, Abbas Kandoro.

Kandoro alifariki dunia Ijumaa usiku katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (NMH) alipokuwa akitibiwa.

Vyanzo vya habari nchini humo vimesema maziko yake yanatarajiwa kufanyika saa 10 jioni Jumapili katika kitongoji anachotokea Ihemi, Iringa Vijijini, mkoani Iringa.

Mwili wa marehemu uliwasili saa 7:30 mchana katika msikiti wa Manyema jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kusaliwa.

Ibada hiyo ya kumuombea marehemu Kandoro ilihudhuriwa na Shehe Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar Zubeiry.

Mbali ya kuongoza Mkoa wa Dar es Salaam, Kandoro aliwahi kuwa mkuu wa mikoa ya Tabora, Arusha, Mwanza na Mbeya, na pia aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Singida.

Kandoro ameacha mjane na watoto watano na wajukuu wanane.

Kandoro alizaliwa Kijiji cha Ihemi, Kata ya Mgamo wilaya ya Iringa Vijijini mkoani Iringa, Septemba 9, 1950.

Katika salamu zake kutokana na kifo hicho, Rais John Magufuli alisema,

“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mkuu wa Mkoa Mstaafu Ndugu Abbas Kandoro, nawapa pole wana familia, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huu, pamoja na wananchi wa mikoa ya Tabora, Arusha, Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya ambako aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa.

“Tumempoteza mtu muhimu ambaye mchango wake katika utumishi kwa umma katika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa halmashauri hautasahaulika.” amesema Rais Magufuli