Mkutano wa kifedha duniani wafanyika mjini Paris, hatua za kusitisha ulipaji deni kwa nchi zilizokumbwa na majanga kutangazwa

Viongozi kadhaa wa dunia wakisikiliza hotuba za ufunguzi wa mkutano kuhusu mkataba mpya wa kifedha duniani mjini Paris, Juni 22, 2023.

Mkuu wa Benki ya Dunia leo Alhamisi anatangaza hatua kadhaa za kusaidia nchi zinazokumbwa na majanga ya asili, ikiwemo kusitisha kwa muda ulipaji wa deni kwa wakopeshaji, wakati viongozi wa dunia wanakutana mjini Paris ili kutoa msukumo wa agenda mpya ya fedha duniani.

Viongozi 40, wakiwemo zaidi ya 10 kutoka Afrika, waziri mkuu wa China na rais wa Brazil, wanakutana katika mji mkuu wa Ufaransa na mashirika ya kimataifa kwenye mkutano kuhusu mkataba mpya wa kifedha duniani na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mkutano huo unalenga kuongeza ufadhili kwa nchi zenye kipato cha chini, kufanya mageuzi kwenye mifumo ya kifedha ya baada ya vita na kutoa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa kufikia maridhiano ya ngazi ya juu kuhusu jinsi ya kuendeleza mipango kadhaa ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto kama ile ya kundi la nchi zilizoendelea kiuchumi (G20) , kongamano la mazingira(COP), IMF na Benki ya dunia na Umoja wa mataifa.