Mkenya Cherono na Mmarekani Ross wasitishwa mashindano mabingwa wa riadha duniani

Lawrence Cherono akiwa jukwani kwa kushinda mbio za Valencia Marathon

Bingwa wa mbio za marathon kutoka Kenya Lawrence Cherono na Mmarekani wa mbio za mita 400 Randolph Ross, wasitishwa kwa muda na kitengo cha uadilifu wanariadha AIU, na hivyo kutoweza kushiriki kwenye mashindano ya riadha yanayoendelea ya mabingwa wa dunia

AIU, inayosimamia masuala ya uadilifu katika riadha ya kimataifa ikiwa ni pamoja na utumiaji wa dawa za kuongeza nguvu, imesema vipimo alivyofanyiwa Cherono vimegundua kwamba ametumia dawa ya aina ya trimetazidine.

Hiyo ni moja kati ya dawa ambazo ziko kwenye orodha ya Idara ya kupambana na dawa za kuongeza nguvu zilizopigwa marufuku kwa mwaka 2022.

Cherono mshindi wa mbio za marathon za Boston na Chicago mwaka 2019, alitoa sampuli ya damu na mkojo wake kabla ya mashindano hapo Mei 23 na kuarifiwa matokeo alipofika Eugene siku ya Alhamisi.

Kwa upande wa Ross, taarifa ya AIU ina sema mwanariadha huyo aliyeshiriki katika timu ya mbio za mita 400 kupokezana iliyoshinda medali ya dhahabu mwaka jana kwenye mashindano ya Olimpiki amesitishwa kutokana na tabia yake wakati wa uchunguzi kuweza kufahamu mahala alikuwepo.

Mashindano yote ya awali ya Marathon na mita 400 yanafanyika Jumapili kwa hivyo hawatoweza kushiriki.